Simbegwire alihuzunika mama yake alipofariki. Baba yake alijitahidi kumtunza mwanaye. Taratibu wakaanza kuwa wenye furaha tena, bila ya Mama Simbegwire. Kila asubuhi walikaa na kupanga mipango ya siku inayofuata. Kila jioni waliandaa chakula cha jioni pamoja. Baada ya kuosha vyombo, baba yake Simbegwire alimsaidia kufanya kazi zake za shule.
Siku moja baba yake Simbegwire alirudi nyumbani kwa kuchelewa. “Mwanangu uko wapi?” aliita. Simbegwire alimkimbilia baba yake. Alisimama ghafla baada ya kumwona baba yake akiwa ameshika mkono wa mwanamke. “Nataka ukutane na mtu muhimu, mwanangu. Huyu ni Anita,” alisema huku akitabasamu.
“Hujambo Simbegwire? Baba yako amenisimulia mengi kukuhusu,” alisema Anita. Lakini hakutabasamu wala kumpa Simbegwire mkono. Baba yake Simbegwire alijaa na furaha. Aliongelea jinsi maisha yatakavyokuwa mazuri watatu hao wakiishi pamoja. “Mwanangu, ni matumaini yangu kuwa utamkubali Anita kuwa mama yako,” alisema.
Maisha ya Simbegwire yakabadilika. Hakuwa na muda tena wa kukaa na baba yake asubuhi. Anita alimpa kazi nyingi za nyumbani zilizomchosha sana kiasi cha kushindwa kufanya kazi zake za shuleni jioni. Alikuwa anaenda moja kwa moja kulala baada ya chakula cha jioni. Faraja pekee aliyokuwa nayo ni blanketi lenye rangi nyingi alilopewa na mama yake. Baba yake Simbegwire hakugundua kwamba binti yake alikuwa hana furaha.
Baada ya miezi michache, baba yake Simbegwire aliwaambia kwamba ana mpango wa kusafiri. “Itanibidi nisafiri kikazi,” alisema. “Lakini najua hakutakuwa na tatizo.” Uso wa Simbegwire ulijawa huzuni, lakini baba yake hakugundua. Anita hakusema lolote. Hakuwa na furaha.
Mambo yakawa mabaya kwa Simbegwire. Aliposhindwa kumaliza kazi au alipolalamika, Anita alimpiga. Wakati wa chakula cha jioni Anita alikula chakula kingi, na kumwachia Simbegwire makombo. Kila usiku Simbegwire alikuwa analia, huku akilikumbatia blanketi la mama yake.
Asubuhi moja, Simbegwire alichelewa kuamka. “Wewe mtoto mvivu,” Anita aliita kwa kelele. Akamvuta Simbegwire kutoka kitandani. Blanketi lake zuri likanasa kwenye msumari na kuchanika vipande viwili.
星卑桂亞超唔開心,佢決定離家出走。佢帶住條毛氈嘅碎片,包咗少少嘢食,沿住爹哋出差嘅路線離開咗屋企。
Simbegwire alikasirika sana. Akaamua kutoroka nyumbani. Akachukua vipande vya blanketi la mama yake. Akachukua na chakula na akaondoka nyumbani. Akaifuata barabara aliyopita baba yake.
Ilipofika jioni alipanda mti mrefu karibu na kijito na akaandaa kitanda kwenye matawi ya mti. Alipokuwa analala akaimba “Maama, maama, maama, umeniacha. Umeniacha na haukurudi tena. Baba hanipendi tena. Mama unarudi lini? Uliniacha.”
Asubuhi iliyofuata, Simbegwire aliimba ule wimbo tena. Wakina mama walipokuja kufua nguo zao walisikia wimbo wa huzuni kutoka kwenye mti mrefu. Wakafikiri ni upepo unatikisa matawi ya mti na wakaendelea na kazi zao. Lakini mama mmoja akasikiliza ule wimbo kwa makini.
Mama huyo akaangalia juu ya mti. Alipomwona msichana na vipande vya blanketi la rangi, akalia, “Simbegwire, mtoto wa kaka yangu!” Wakina mama wengine wakaacha kufua na wakamsaidia Simbegwire kushuka toka juu ya mti. Shangazi yake akamkumbatia na kumfariji.
Shangazi yake Simbegwire akampeleka nyumbani kwake. Akampatia chakula, akampeleka kitandani na akamfunika na blanketi la mama yake. Usiku ule Simbegwire akalia alipokwenda kulala. Lakini yalikuwa machozi ya furaha. Alijua shangazi yake atamtunza.
Baba yake Simbegwire aliporudi nyumbani, alikikuta chumba chake kikiwa tupu. “Nini kimetokea, Anita?” aliuliza kwa simanzi. Anita akaelezea kuwa Simbegwire alitoroka. “Nilitaka aniheshimu,” alisema. “Labda nilikuwa mkali sana.” Baba yake Simbegwire aliondoka nyumbani na akaelekea kwenye kijito. Akaenda kwenye kijiji cha dada yake kuuliza kama amemwona Simbegwire.
Simbegwire alikuwa anacheza na binamu zake alipomwona baba yake akija kwa mbali. Aliogopa kuwa baba yake angekuwa amekasirika, na akakimbilia ndani ya nyumba ili ajifiche. Baba yake alimwendea na akamwambia, “Simbegwire umempata mama mzuri. Anayekupenda na kukuelewa. Najivunia kuwa nawe na ninakupenda.” Walikubaliana kuwa Simbegwire angeishi na shangazi yake kwa muda wote atakaotaka.
Baba yake alikuwa akimtembelea kila siku. Mwishoe akaja na Anita. Akampa mkono Simbegwire. “Nisamehe, nilikosea,” akalia. “Utanipa nafasi kujaribu tena?” Simbegwire alimwangalia baba yake aliyekuwa na uso wa wasiwasi. Baadaye akamwendea Anita taratibu na akamkumbatia.
Wiki iliyofuata, Anita aliwaalika Simbegwire, binamu zake, na shangazi yake kwa ajili ya chakula. Anita akaandaa vyakula vyote ambavyo Simbegwire anavipenda, na kila mmoja akala hadi akashiba. Baada ya kula watoto wakaenda kucheza huku watu wazima wakiongea. Simbegwire akajisikia furaha na jasiri. Akaamua kuwa si muda mrefu atarejea nyumbani kuishi na baba yake na mama yake wa kambo.