Kituo kidogo cha mabasi kijijini mwetu kilijaa shughuli za watu na mabasi. mabasi mengi yalikuwa yamejaa mizigo. Chini, palikuwa na mizigo zaidi ya kupakia. Makondakta walikuwa wanataja majina ya sehemu mabasi yalikokuwa yanaelekea.
Basi la kwenda mjini lilikaribia kujaa, lakini watu wengine walikuwa wanasukumana kupanda. Baadhi yao walipakia mizigo chini ya basi. Wengine waliiweka katika sehemu ya juu.
Nilijipenyeza ndani na kukaa karibu na dirisha. Mtu aliyeketi karibu nami alishika mfuko wa plastiki wa kijani kibichi. Alivaa viatu vilivyochakaa, koti kuukuu na alionekana kuwa na wasiwasi.
Upakiaji mizigo ulikamilika na abiria wakawa wameketi. Wachuuzi walizidi kusukumana kutaka kuingia ndani ya basi ili wauze bidhaa zao. Kila mmoja alitaja kwa sauti majina ya bidhaa alizokuwa anauza. Maneno yao yalinifurahisha.
Wachuuzi walisukumana huku wakitafuta njia ya kushuka. Wengine waliwarudishia wasafiri chenji zao. Wengine walifanya juhudi za mwisho kuuza bidhaa zao.
Lakini mawazo yangu yalirejea nyumbani. Je, mamangu atakuwa salama? Je, sungura wangu wataleta hela zozote? Je, ndugu yangu atakumbuka kunyunyizia maji miche ya miti yangu?
Basi la kurudi lilikuwa linajaa upesi. Muda mfupi baadaye, lingeanza safari ya kwenda mashariki. Jambo la maana kwangu wakati huo lilikuwa kuanza kutafuta nyumba ya mjomba wangu.